|
Katika Wilaya ya Same kumekuwepo na Mashirika kadhaa, ama yaliyoanzishwa
humu Wilayani au toka nje yaliyo ya Kimataifa; yanayojishughulisha
na Maendeleo. Hata kabla ya Mashirika hayo kuanzishwa ama kuingia
Wilayani - yalikuwepo Mashirika ya dini - mfano Waislamu na Wakristo.
Wao hawakuhubiri dini zao tu, bali walianzisha kazi mbalimbali
za maendeleo, hasa Afya na Elimu na kazi nyingine za maendeleo.
Mashirika hayo, kila moja lilifanya kazi zake bila kuwa na uhusiano
kati yao. Katika hali hii ndipo kukatokea watu fulani na wazo
kwamba ni kwa jinsi gani Mashirika husika yanaweza kushirikiana?
Na je ushirikiano huo uwe wa jinsi gani?
SANGO ikaundwa , Julai 1999, Mkutano Mkuu ukafanyika - ambao
ulichagua Mwenyekiti - Bwana Dismas Nyaki, Makamu Mwenyekiti akiwa
ni Bwana Mbwambo. Pamoja na viongozi hao, kulichaguliwa Halmashauri
Kuu yenye watu 12. Halmashauri Kuu hufanya kazi kwa muda wa miaka
mitatu.
SANGO ilisajiliwa kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hii
Januari 2000; na mwezi Machi mwaka huo huo - Mkutano Mkuu wa pili
ulifanyika, wajumbe wake walikuwa ni kutoka Mashirika yaliyo wanachama.
Mkutano huo uliunda Kamati ambazo ni:-
Afya
Kilimo / Mali Asili
Elimu
Jinsia
Masoko
Wajumbe wa kila Kamati hutokana na Mashirika yaliyo Wanachama
- ambao kila Kamati haizidi watu kumi. Hawa hutegemea kazi wafanyazo
katika Mashirika wanakotoka.
Ili kuiwezesha SANGO iwe na dira ya kazi mwaka 2000, kulifanyika
warsha tena iliyoweka mkakati wa miaka mitatu. Kwenye miaka hiyo,
ni kuiwezesha SANGO kuhudumia Mashirika Wanachama.
Kusudi Mashirika Wanachama yaweze kufanya kazi vizuri kwa Jamii
- SANGO inapaswa kuyajengea uwezo kwa njia ya mafunzo. Pia kushawishi
na kujenga mazingira mazuri huko kwenye Jamii, ambapo, Mashirika
yanafanya kazi za kimaendeleo. Tena kusaidia Mashirika kuweka
kumbukumbu na taarifa zao vizuri; pia kupitia taarifa na kumbukumbu
kwenye Ofisi. Kutokana taarifa hizo - SANGO itaona ni wapi pa
kushauri.
Kwa mujibu wa Mratibu wa SANGO - Bwana Essore Maregeri Essore
alisema, "Mpango wa kwanza wa miaka 3 uliishia Desemba 2003;
ukihusu kuimarisha SANGO na Sekretarieti yake kusudi iweze kuhudumia
Mashirika, Wanachama wake vizuri zaidi na hata Wananchi kwa ujumla"
Kwa vile mpango wa kwanza wa miaka mitatu, uliisha mwishoni
mwa mwaka (2003). Na kwamba mpango mwingine wa miaka 3 haujaandaliwa,
lakini utalenga jinsi SANGO itakavyosaidia Mashirika wanachama;
kusudi kwa upande wao, waweze kufanya kazi za maendeleo kwa ufanisi.
Mpango utaanzia mwaka huu (2006).
Mratibu alisema "SANGO imeweka mpango wa kutembelea kila
Kijiji kwenye Wilaya hii itakavyowezekana; kutoa elimu ya uraia
ili Jamii itambue haki zao na ili waweze kuwajibisha Viongozi
wao, kuanzia Vijijini, Wilaya hata Taifani; waonapo kuwa mambo
hayaendi vizuri"
Akaongeza kuwa kazi hiyo inatarajiwa ianze katika mwaka huu wa
fedha; kusudi ifikapo wakati wa uchaguzi mkuu mwakani (2006),
watu wawe wameelimika vya kutosha - ili wachague viongozi bora.
Kwa kuanzia Sango ilianzisha midahalo na kushirikisha wananchi
wa vijiji kutoka Kata sita katika Wilaya hii kwa majadiliano juu
ya mkakati wa kuondoa umasikini na kuto fursa kwa wananchi kutoa
mawazo yao juu ya mkakati wa pili unaoandaliwa na ofisi ya makamu
wa Raisi.
Washiriki kwenye vikao hivyo walitoa mawazo kama walivyoona yalisaidia
kuboresha, na yale yatakayosaidia siku za baadae. Kwa upande wa
afya, washiriki walisema kwamba, juhudi ziongezwe kusudi kila
Hospitali, Vituo vya Afya visivyo na Vyandarau vipatiwe. Na kuwe
na Madaktari Watalam katika Hospitali.
Kuhusu Kilimo wanasema kwamba pembejeo zipatikane kwa wakati
muafaka na kwa bei nafuu, pamoja na kupatikana kwa masoko kuwezesha
Wakulima kuuza mazao yao. Hii ni mifano michache kati ya yote
yaliyojitokeza Jamii iliposhirikishwa. Hivyo mawazo hayo yametumwa
katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kusudi yafahamike.
Same Association of Non-Governmental Organisation (Mtandao wa
Mashirika yasiyo ya Kiserikali Wilayani Same) inayo Mashirika
wanachama 40. Haya Mashirika wanachama hutoa kiingilio na ada
ya kila mwaka. Mashirika yamepangwa katika makundi manne kufuatana
na hali ya Shirika lilivyo. Na kiingilio hata ada hutegemea hali
ilivyo.
Viwango ni kama ifuatavyo:-
Wapo wanaolipa
Sh. 10,000/=
Sh. 20,000/=
Sh. 30,000/=
Sh. 40,000/=
"Pamoja na kuwa Mashirika huhitajiwa kulipa kiingilio na
ada ya kila mwaka; lakini sio yote yenye uwezo. Tena kuna mengine
yaliyokuwa na mawazo kwamba, kuwa mwanachama SANGO ndiyo itakayowasaidia
kifedha, lakini ilipoonekana kwamba ni kinyume chake kulipa hupungua,"
Mratibu aliongeza
Njia nyingine za mapato ni kutoka Mashirika ya Kimataifa na
ya humu nchini yasiyo ya Kiserikali na mengine yanayoshirikiana
kwenye kazi - mfano VECO Tanzania. Wafadhili wengene ni PAMOJA
iliyo na Ofisi Moshi, TANGO na Ofisi ya Makamu wa Rais. Kunapotokea
mpango fulani wa kipekee, hutafutiwa Mfadhili ambaye mwelekeo
wake hukubaliana na mradi unaokusudiwa.
|